Genesis 41

Ndoto Za Farao

1 aBaada ya miaka miwili kamili kupita, Farao aliota ndoto: Tazama alikuwa amesimama kando ya Mto Naili, 2 bwakati ngʼombe saba, wazuri na wanono, walitokea mtoni wakajilisha kwenye matete. 3Baada yao ngʼombe wengine saba, wabaya na waliokonda, wakatokea mtoni Naili wakasimama kando ya wale wanono ukingoni mwa mto. 4 cWale ngʼombe wabaya na waliokonda wakawala wale saba wazuri na wanono. Kisha Farao akaamka.

5Farao akaingia usingizini tena akaota ndoto ya pili: Akaona masuke saba ya nafaka, yenye afya na mazuri, yanakua katika bua moja. 6 dBaadaye, masuke mengine saba yakachipua, yakiwa membamba yaliyonyaushwa na upepo wa mashariki. 7 eMasuke yale membamba yakameza yale masuke saba yenye afya na yaliyojaa. Basi Farao akaamka kutoka usingizini, kumbe ilikuwa ndoto.

8 fAsubuhi yake, alifadhaika akilini, hivyo akawaita waaguzi wote pamoja na watu wenye busara wa Misri. Walipokuja, Farao akawaeleza ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumfasiria.

9Ndipo mnyweshaji mkuu alipomwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kuhusu kosa langu. 10 gWakati fulani Farao aliwakasirikia watumishi wake, akanifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa ulinzi. 11 hKila mmoja wetu aliota ndoto katika usiku mmoja na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti. 12 iBasi kijana wa Kiebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, alikuwa mtumishi wa mkuu wa kikosi cha ulinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupa kila mtu tafsiri ya ndoto yake. 13 jNayo mambo yakawa sawa kabisa na jinsi alivyotufasiria ndoto zetu: Mimi nilirudishwa kazini mwangu na huyo mtu mwingine akaangikwa.”

14 kBasi, Farao akatuma Yosefu aitwe, naye akatolewa kifungoni haraka. Baada ya kunyoa na kubadilisha nguo zake akaenda mbele ya Farao.

15 lFarao akamwambia Yosefu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia ikisemwa kwa habari yako kwamba unapoelezwa ndoto waweza kuifasiri.”

16 mYosefu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.”

17Kisha Farao akamwambia Yosefu, “Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa Mto Naili, 18nikawaona ngʼombe saba, wazuri na wanono, wakijitokeza kutoka mtoni wakaja kujilisha kwenye matete. 19Baada ya hao, ngʼombe wengine saba wadhaifu wakatokea, wabaya sana na waliokonda. Kamwe sikuwahi kuona ngʼombe wabaya jinsi hiyo katika nchi yote ya Misri. 20Hao ngʼombe waliokonda na wabaya sana wakawala wale ngʼombe saba walionona waliojitokeza kwanza. 21Lakini hata baada ya kuwala, hakuna mtu ambaye angeweza kusema kwamba wamekula, bado walionekana wabaya kama mwanzoni. Kisha nikaamka kutoka usingizini.

22“Pia katika ndoto zangu niliona masuke saba ya nafaka, yamejaa na mazuri, yanakua katika bua moja. 23Baada ya hayo masuke mengine saba yakachipua, yaliyonyauka, membamba na yamekaushwa na upepo wa mashariki. 24Yale masuke membamba ya nafaka yakayameza yale masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka. Nimewaeleza waaguzi, wala hakuna yeyote aliyeweza kunifasiria.”

25 nNdipo Yosefu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni ndoto iyo hiyo moja. Mungu amemfunulia Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. 26Ngʼombe saba wazuri ni miaka saba, nayo masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka ni miaka saba, ni ndoto iyo hiyo moja. 27Ngʼombe saba waliokonda na wabaya wale waliojitokeza baadaye ni miaka saba, vivyo hivyo masuke saba ya ngano yaliyodhoofika na kukaushwa na upepo wa mashariki, ni miaka saba ya njaa.

28“Ni kama vile nilivyomwambia Farao: Mungu amemwonyesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. 29 oMiaka saba ya neema inakuja katika nchi yote ya Misri, 30 plakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo neema yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi.

31“Neema iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. 32Sababu ya ndoto kumjia Farao kwa namna mbili ni kwamba jambo hilo Mungu ameshaamua kwa hakika, naye Mungu atalifanya karibuni.

33 q“Basi sasa Farao na atafute mtu mwenye akili na hekima ili amweke kuwa msimamizi wa nchi ya Misri. 34 rFarao na aweke wenye amri nchini kote wakusanye sehemu ya tano ya mavuno ya Misri katika miaka hii saba ya neema. 35 sWakusanye chakula chote katika miaka hii saba ya neema inayokuja na kuhifadhi nafaka chini ya mamlaka ya Farao, iwe akiba ya chakula katika miji. 36Chakula hiki kitakuwa akiba ya tahadhari kwa ajili ya nchi, ili kitumike katika ile miaka saba ya njaa itakayokuja Misri, ili nchi isiharibiwe na njaa.”

37Mpango huu ulionekana mzuri kwa Farao na kwa maafisa wake wote. 38 tHivyo Farao akawauliza, “Je tunaweza kumpata yeyote kama mtu huyu, ambaye Roho wa Mungu yumo ndani yake?”

39Ndipo Farao akamwambia Yosefu, “Maadamu Mungu amekufunulia yote haya, hakuna mwingine yeyote mwenye akili na hekima kama wewe. 40 uWewe utakuwa msimamizi wa jumba langu la kifalme, na watu wangu wote watatii amri zako. Ni kuhusu kiti cha ufalme tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”

Yosefu Msimamizi Wa Misri

41 vKwa hiyo Farao akamwambia Yosefu, “Sasa nakuweka uwe msimamizi wa nchi yote ya Misri.” 42 wNdipo Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kidoleni mwake na kuivalisha katika kidole cha Yosefu. Akamvika majoho mazuri ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni mwake. 43 xAkampandisha katika gari lake la farasi kama msaidizi wake, watu wakatangulia wakishangilia, wakisema, “Fungueni njia!” Ndivyo Farao alivyomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri.

44Kisha Farao akamwambia Yosefu, “Mimi ni Farao, lakini pasipo neno lako, hakuna mtu mwenye ruhusa kuinua mkono au mguu katika nchi yote ya Misri.” 45 yFarao akamwita Yosefu Safenath-Panea, pia akampa Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni,
Yaani Heliopoli (Mji wa Jua).
kuwa mke wake. Ndipo Yosefu akaitembelea nchi yote ya Misri.

46 aaYosefu alikuwa na miaka thelathini alipoingia katika utumishi wa Farao mfalme wa Misri. Naye Yosefu akatoka mbele ya Farao akasafiri katika nchi yote ya Misri. 47 abKatika ile miaka saba ya neema nchi ilizaa mazao kwa wingi sana. 48 acYosefu akakusanya chakula chote kilichozalishwa katika ile miaka saba ya neema nchini Misri, akakihifadhi katika ghala za miji. Katika kila mji kulihifadhiwa chakula kilichozalishwa katika mashamba yaliyouzunguka mji huo. 49 adYosefu alihifadhi nafaka nyingi, mfano wa mchanga wa bahari, ilikuwa nyingi mno kiasi kwamba walishindwa kuweka kumbukumbu kwa sababu akiba ilizidi sana kupita kipimo.

50Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, alikuwa amemzalia Yosefu wana wawili wa kiume. 51 aeYosefu akamwita mzaliwa wake wa kwanza Manase, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote pamoja na jamaa yote ya nyumba ya baba yangu.” 52 afMwana wa pili akamwita Efraimu, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenistawisha katika nchi ya mateso yangu.”

53Ile miaka saba ya neema huko Misri ikaisha, 54 agnayo miaka ile saba ya njaa ikaanza, sawasawa na alivyosema Yosefu. Kulikuwa na njaa katika nchi nyingine zote, bali katika nchi yote ya Misri kulikuwa na chakula. 55Wakati nchi yote ya Misri ilipopatwa na njaa, watu wakamlilia Farao ili awape chakula. Ndipo Farao alipowaagiza Wamisri wote, akisema, “Nendeni kwa Yosefu, nanyi mfanye anachowaambia.”

56Wakati njaa ilipokuwa imeenea katika nchi yote, Yosefu akafungua ghala za vyakula na kuwauzia Wamisri nafaka, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno katika nchi yote ya Misri. 57Pia nchi nyingine zote zilikuja Misri kununua nafaka kutoka kwa Yosefu, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno duniani kote.

Copyright information for SwhNEN